Jumamosi 7 Novemba 2026 - 23:48
Ayatullah Arafi Afafanua Sifa Sita Muhimu za Khutba ya Fadaki na Masharti ya Wanafunzi wa Hawza Kutekeleza Wajibu Wao wa Kimataifa Usio na Mipaka ya Kijiografia

Mkuu wa Hawza nchini Iran, Ayatullah Arafi, akizungumzia nafasi ya mwanafunzi wa elimu za kidini na jukumu kubwa lililo mabegani mwake, amesisitiza kuwa: “Kazi mliyoibeba ni kubwa mno na yenye thamani kubwa, hivyo haipaswi kuichukulia kijuujuu wala kuiona kuwa ni jambo dogo.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza Arafi, asubuhi ya leo, alitembelea Hawza ya Sayyidush-Shuhadaa (a.s) iliyopo Qum Iran. Mwanzoni mwa ziara hiyo, msimamizi wa Hawza hiyo pamoja na wasaidizi wake waliwasilisha ripoti kuhusu shughuli za kielimu na za utafiti zinazofanyika katika kituo hicho.

Akizungumza mbele ya walimu na wanafunzi wa Hawza hiyo, Mkuu wa Hawza alizungumzia nafasi ya kituo hicho katika tathmini zinazofanywa na uongozi wa Hawza, akisema: “Hawza ya Sayyidush-Shuhadaa (a.s) ni miongoni mwa Hawza nzuri na zilizofanikiwa, ambazo katika tathmini zilizofanyika zimetambuliwa kuwa ni miongoni mwa Hawza zinazostahili pongezi na kuthaminiwa.”

Mjumbe wa Baraza la Mafakihi katika Baraza la Walinzi wa Katiba Iran, alisema kuwa; uwepo wake katika Hawza hiyo ni fursa ya kuthamini juhudi zinazofanywa na jumuiya hiyo. Aliongeza: “Katika fursa hii, napenda kutoa shukrani na pongezi zangu za dhati kwa wanafunzi wapendwa wa elimu za kidini ambao, Inshaallah, watakuwa nguzo za mustakabali wa Hawza na waenezaji wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu nchini Iran na duniani kote.”

Ayatullah Arafi, akiendelea kuzungumzia kazi za kitaaluma na vitabu vilivyowasilishwa katika Hawza hiyo, alieleza kuwa; kuwafahamisha wanafunzi urithi wa kielimu na kazi za wanazuoni wakubwa wa zama zilizopita ni hatua yenye thamani kubwa. Alibainisha kuwa: “Kufahamu urithi wa kielimu na kiutamaduni wa waliotutangulia ni njia ya kunufaika na hazina yao adhimu ya maarifa, sambamba na kuwa msingi wa kufanya tafiti na uchunguzi wa kielimu katika siku zijazo. Hatua hii inastahili kuthaminiwa na kupongezwa.”

Khutba ya Fadakiyya ni miongoni mwa matini za kale na zenye mamlaka katika historia ya Uislamu

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alielekeza fikra zake katika sehemu ya Khutba ya Fadakiyya ya Bibi Fatimah Zahraa (s.a), akizungumzia nafasi yake ya kihistoria na uaminifu wa mapokezi yake. Alisema: “Bila shaka, Khutba ya Fadakiyya ni miongoni mwa matini zenye mamlaka na marejeo muhimu katika historia ya Uislamu. Khutba hii imenukuliwa katika vitabu vya wanazuoni wa madhehebu ya Ahlu Sunna na vilevile katika vitabu vya wanazuoni wa madhehebu ya Shia.”

Mkuu wa Hawza nchini Iran, akizungumzia jinsi Khutba ya Fadakiyya ilivyonukuliwa katika vitabu vya wanazuoni wa Ahlu Sunna, alisema: “Miongoni mwa marejeo muhimu yaliyonukuu khutba hii ni kitabu cha Tabaqatun-Nisaa, kilichoandikwa na mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Ahlu Sunna, ambamo maandishi mazuri ya Khutba ya Fadakiyya yamehifadhiwa. Mbali na kitabu hicho, khutba hii pia imezingatiwa katika marejeo mengine mengi ya Shia na Ahlu Sunna, pamoja na baadhi ya vitabu vinavyotegemewa na marejeo asilia ya Kiislamu.”

Mjumbe wa Mafakihi wa Baraza la Walinzi wa Katiba, akibainisha kuwa; Khutba ya Fadakiyya ilikuwa tayari imepata umaarufu na nafasi ya pekee tangu miaka ya mwanzo baada ya kutolewa kwake, alisema: “Baadhi ya wanazuoni wameeleza nafasi ya khutba hii kwa kusema kuwa; maandishi ya Khutba ya Fadakiyya, kama sehemu ya urithi wa fikra na itikadi za madhehebu ya Shia, yalikuwa yakihifadhiwa katika nyumba za Mashia. Familia za Kishia zilikuwa zikijitahidi kuhakikisha kuwa mkusanyiko huu wa fikra na katiba pana ya maarifa ya Mwenyezi Mungu vinapitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, vinawafundisha watoto wao na kuviweka katika mfumo wao wa elimu na mafunzo.”

Alisema kuwa; nafasi hiyo ya kihistoria ni ishara ya msingi imara wa uaminifu na umuhimu wa Khutba ya Fadakiyya huku akisisitiza: “Sisi pia tunapaswa kuwa na mazoea ya kuisoma na kuizingatia khutba hii yenye thamani kubwa, pamoja na kujitahidi kuyafahamu na kuyafafanua mafundisho yake.”

Sifa sita muhimu za Khutba ya Fadakiyya

1. Kiwango cha juu kabisa cha ufasaha na balagha

Mkuu huyo wa Hawza akifafanua sifa za Khutba ya Fadakiyya, aliitaja sifa yake ya kwanza kuwa ni kufikia kiwango cha juu kabisa cha ufasaha na balagha, alisema: “Miongoni mwa matini za fasihi, historia na mapokezi ya lugha ya Kiarabu, Khutba ya Fadakiyya inashikilia nafasi ya juu sana, ni miongoni mwa matini zilizofikia kilele cha ufasaha na balagha.”

Mjumbe wa Mafakihi wa Baraza la Walinzi wa Katiba, akizungumzia namna wanazuoni walivyozingatia maneno na khutba za wanawake mashuhuri katika historia ya Uislamu, alisema: “Katika baadhi ya vitabu vya fasihi, vikiwemo kitabu cha Balaghaatun-Nisaa, yamekusanywa maneno na khutba za wanawake waliokuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza kwa ufasaha na balagha. Hata hivyo, Khutba ya Fadakiyya ina nafasi iliyo juu zaidi ya kuwa tu kazi ya kifasihi iliyotolewa na mwanamke Muislamu, ni miongoni mwa matini asilia na bora za fasihi ya Kiislamu. “Bila shaka, Khutba ya Fadakiyya inastahili kuwekwa pamoja na Nahjul-Balagha na maneno ya Mtume Mtukufu wa Uislamu (s.a.w.w). Kwa upande wa kiwango cha ufasaha na balagha, ni miongoni mwa matini bora na za daraja la kwanza katika ulimwengu wa Kiislamu.”

Mkuu wa Hawza akisisitiza kuwa; ukubwa wa kifasihi wa khutba hii hauishii katika madhehebu au kundi fulani, alisema: “Ufasaha na balagha ya Khutba ya Fadakiyya vinavuka mipaka ya tofauti za kimadhehebu na kijinsia. Khutba hii ni matini tajiri sana ya kifasihi yenye uimara mkubwa na muundo bora wa lugha ya Kiarabu. Inaweza kuhesabiwa miongoni mwa kazi bora na za daraja la kwanza za fasihi ya Kiarabu.”

Ayatullah Arafi, akizungumzia uzuri wa kifasihi wa khutba hii, alisema: “Watu wanaoifahamu lugha ya Kiarabu, msamiati wake na undani wa vipengele vyake vya kifasihi, na ambao wamejijengea kipaji cha kifasihi, wanaposoma Khutba ya Fadakiyya hufurahia uzuri wake, umahiri wake na mvuto wake wa kipekee. Kwa upande wa matumizi ya mbinu za kifasihi, miundo ya lugha na namna ya uwasilishaji wa ujumbe, khutba hii ni kazi bora mno inayostahili kutafakariwa kwa kina.”

2. Kina cha maarifa na undani wa maudhui

Alitaja sifa ya pili ya Khutba ya Fadakiyya kuwa ni kina cha maarifa na undani wa maudhui yake, akisema: “Tunapoichunguza khutba hii kwa makini, tunabaini kuwa kila mahali ambapo Bibi Fatimah Zahraa (s.a) alipoingia katika mjadala fulani, aliwasilisha maarifa ya kina kabisa na fikra sahihi na nyeti zaidi, akizifafanua kwa wasikilizaji kwa lugha imara na ya kitaaluma.”

Mkuu wa Hawza aliendelea kusema: “Usahihi na undani wa kielimu na kimaarifa unaojitokeza katika khutba hii yote ni wa kiwango cha ajabu, katika kazi hii, kuanzia mijadala ya kina ya elimu ya itikadi na misingi ya imani, hadi masuala ya kifiqhi na kisheria yanayohusiana na suala la Fadak, yote yamewasilishwa kwa umakini na uimara wa hali ya juu.”

Ayatullah Arafi, akieleza kuwa suala la Fadak halikuwa tu suala la mali na sheria, alisema: “Bibi Fatimah Zahraa (s.a), alipokuwa akifafanua suala la Fadak, aliwasilisha mijadala na maarifa yenye kina kikubwa zaidi, jambo hili ndilo lililoifanya Khutba ya Fadakiyya kuwa na nafasi ya pekee katika upande wa kina cha maarifa na maudhui.”

3. Ukamilifu wa maudhui na uwasilishaji wa picha pana ya fikra za Kiislamu

Aliutaja ukamilifu wa maudhui kuwa ni sifa ya tatu muhimu ya Khutba ya Fadakiyya, akisema: “Khutba hii ni miongoni mwa khutba na nyaraka chache za kihistoria zenye thamani kubwa katika urithi wa Kiislamu, ambazo zimekusanya sehemu pana za mfumo wa fikra za Uislamu.”

Mkuu wa Hawza aliongeza kusema: “Katika khutba hii, kwanza kunajadiliwa misingi ya utambuzi na kumjua Mwenyezi Mungu, kisha maarifa hayo yanaelekezwa katika masuala muhimu kama Uimamu, Wilaya ya Mwenyezi Mungu na misingi mikuu ya kiitikadi. Baadaye, khutba hii inazungumzia pia masuala muhimu ya kisiasa na kijamii yaliyokuwa yakikabili jamii ya Kiislamu katika kipindi hicho.”

Ayatullah Arafi, akisisitiza kuwa Khutba ya Fadakiyya inatoa picha pana ya fikra za Kiislamu, alisema: “Ikiwa mtu atataka kufahamu mfumo wa fikra za Uislamu kupitia kozi moja ya kielimu, anaweza kupata dalili na misingi mikuu ya mfumo huo kwa kuisoma na kuichunguza kwa makini Khutba ya Fadakiyya, hii ni kwa sababu kanuni na misingi muhimu ya fikra za Kiislamu imefafanuliwa ndani ya khutba hii na kuwekwa mbele ya jamii na wanadamu wote.”

Alisema kuwa sifa tatu za kwanza za Khutba ya Fadakiyya ni kuwa na kiwango cha juu cha ufasaha na balagha, kina cha maarifa na maudhui, pamoja na ukamilifu katika kufafanua mfumo wa fikra za Uislamu. Akasisitiza: “Kukusanyika sifa hizi tatu katika matini moja ya kihistoria, kielimu na kifasihi ni ishara ya ukubwa na nafasi ya kipekee ya Khutba ya Fadakiyya.”

4. Nafasi yake ya kihistoria na uwezo wake wa kuleta mabadiliko

Mkuu huyo wa Hawza, akiendelea na maelezo yake, akiitaja nafasi yake ya kihistoria na uwezo wake wa kuleta mabadiliko kuwa ni sifa ya nne ya Khutba ya Fadakiyya. Alisema: “Khutba hii ni kama katiba ya kufafanua mojawapo ya nyakati muhimu na nyeti sana katika historia ya Uislamu, ambayo ilikuwa na matukio yaliyobeba mustakabali wa jamii ya Kiislamu.”

Khutba ya Fadakiyya: Katiba ya mabadiliko katika kipindi muhimu cha historia ya Uislamu

Ayatullah Arafi, akizungumzia mazingira ya kihistoria yaliyosababisha kutolewa kwa Khutba ya Fadakiyya, alisema: “Khutba hii inapaswa kuchukuliwa kuwa ni katiba ya mabadiliko katika kipindi muhimu cha historia ya Uislamu; kipindi ambacho masuala ya msingi na yaliyobeba mustakabali wa jamii ya Kiislamu yalikuwa yakiibuliwa. Katika kipindi hicho, Bibi Fatimah Zahraa (s.a), kwa kufafanua maarifa ya kina na kuweka wazi misimamo yake, aliiachia historia ya Uislamu ukweli muhimu ambao hautasahaulika.”

Khutba ya Fadakiyya ni katiba ya kulinda Uimamu na kuendeleza njia ya kweli ya Utume wa Mtume (s.a.w.w)

Ayatullah Alireza Arafi, akifafanua nafasi ya kihistoria na kimaarifa ya Khutba ya Fadakiyya, aliitaja khutba hii yenye nuru kuwa ni katiba ya kulinda njia ya Uimamu na kuendeleza kwa usahihi Utume wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w).

Alisema: “Katika kipindi nyeti ambacho kulikuwa na dhana kwamba njia ya Uimamu na mwendelezo wa Utume ulikuwa unakaribia kuzimika, Bibi Fatimah Zahraa (s.a), kupitia ushujaa wake wa kujitokeza na hotuba yake iliyofungua macho ya watu, alibadilisha mwelekeo wa mambo na hakuruhusu njia hii ya Mwenyezi Mungu isahaulike.”

Akiizungumzia nafasi ya kihistoria ya wanawake watatu wakubwa katika Uislamu, yaani Bibi Khadija Kubra (s.a), Bibi Fatimah Zahraa (s.a) na Bibi Zaynab Kubra (s.a), alisema: “Katika historia ya Uislamu kuna vipindi nyeti ambapo madhehebu ya haki yalikabiliwa na migogoro mikubwa. Wakati mwingine hali ilifikia hatua ambayo ilionekana kana kwamba mifumo yote ya mambo ilikuwa imesambaratika na hakuna tena njia ya kuendeleza safari. Hata hivyo, katika mazingira kama hayo, wanawake hawa watatu wakubwa walijitokeza kama mashujaa na viongozi wa historia ya Uislamu, na kubadilisha mwelekeo wa matukio.”

Wanawake watatu wakubwa wa Uislamu: Mashujaa wa vipindi vilivyoamua mustakabali wa historia

Mkuu wa Hawza akieleza kuwa; Bibi Khadija (s.a), Bibi Fatimah Zahraa (s.a) na Bibi Zaynab (s.a) walitekeleza majukumu muhimu katika vipindi vitatu nyeti vya historia ya Uislamu, alisema: “Wanawake hawa watatu wakubwa, katika nyakati za mabadiliko makubwa na mazingira ambayo Uislamu na upande wa haki ulikabiliwa na migogoro mikubwa, walikuwa na nafasi za kuamua mwelekeo wa matukio. Kwa imani yao, uelewa wao wa kina, ushujaa na msimamo thabiti, waliweza kubadilisha hali ya mambo ilivyoonekana kwa nje.”

Akizungumzia nafasi ya Bibi Khadija Kubra (s.a) katika mwanzo wa Utume wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w), alisema: “Wakati Mtume Mtukufu (s.a.w.w) alipoanza kutekeleza Utume wake wa Mwenyezi Mungu, na watu wengi walikuwa bado hawajamuamini, Bibi Khadija (s.a) alisimama pamoja na Mtume na malengo yake matakatifu. Kwa mujibu wa kauli iliyonukuliwa kutoka kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w), katika kipindi ambacho watu wengine walikuwa wamemwacha Mtume peke yake, Bibi Khadija (s.a) alikuwa pamoja naye na akimpa msaada na kumuunga mkono katika Utume wake wa Mwenyezi Mungu.”

Ayatullah Arafi aliendelea kusema: “Vilevile, Bibi Fatimah Zahraa (s.a), baada ya kufariki dunia Mtume Mtukufu (s.a.w.w), alitekeleza jukumu lisilo na mfano katika mazingira ambayo jamii ya Kiislamu ilikuwa imekabiliwa na mabadiliko na migogoro mikubwa. Khutba ya Fadakiyya na kujitokeza kwake kihistoria katika Msikiti wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w) ni ushahidi ulio wazi kuwa, katika kipindi nyeti zaidi cha historia ya Uislamu, alijitokeza kwa ajili ya kutetea ukweli, Uimamu na kuendeleza njia ya Utume.”

Mjumbe wa Mafakihi wa Baraza la Walinzi wa Katiba, akizungumzia nafasi ya Bibi Zaynab Kubra (s.a) baada ya tukio la Ashura, alisema: “Ikiwa tutayachambua kwa usahihi matukio yaliyotokea baada ya adhuhuri ya siku ya Ashura, kwa mtazamo wa kwanza hatutaona mwanya wowote wa matumaini. Inaonekana kana kwamba njia zote zimefungwa na njia ya Wilaya na Uimamu imefikia mwisho wake. Hata hivyo, Bibi Zaynab Kubra (s.a), katika mazingira hayo hayo, alikuwa mfano wa matumaini, ustahimilivu na mtazamo wa mbali kuhusu mustakabali.”

Bibi Zaynab (s.a): Aliyebadilisha mandhari ya nje ya kutekwa na kuwa uwanja wa nguvu ya kiroho

Mkuu wa Hawza akifafanua mazingira aliyokuwa nayo Bibi Zaynab (s.a) katika baraza la Ubaydullah bin Ziyad na Yazid, alisema: “Kwa mwonekano wa nje, mazingira yalikuwa yamechorwa kana kwamba Bibi Zaynab (s.a) na watu waliokuwa pamoja naye walikuwa mateka, huku maadui wakijiona kuwa washindi wa moja kwa moja. Upande mmoja walikuwepo mateka waliokuwa mikononi mwa maadui, na upande mwingine walikuwepo watu waliokuwa na nguvu na uwezo wa kimwili na mali kwa mwonekano wa nje.”

Aliongeza: “Mtu mwenye mtazamo wa kina na unaozingatia ukweli atatambua kuwa uhalisia wa tukio hilo ulikuwa tofauti kabisa. Ushujaa na ukubwa wa nafsi ya Bibi Zaynab (s.a), licha ya kuwa katika kilele cha utumwa wa mateka, misiba na matatizo, ulikuwa mkubwa kiasi cha kubadilisha taswira halisi ya nguvu. Kwa namna ambayo mtu akilitazama baraza hilo kwa jicho la ukweli, atatambua kuwa wenye majumba makubwa na nguvu za nje ndio waliokuwa mateka mbele ya utukufu na mamlaka ya kiroho ya Bibi Zaynab (s.a).”

Ayatullah Arafi alisisitiza: “Hii ndiyo roho inayoweza kuubadilisha ulimwengu. Ulimwengu wote haujajengwa kwa mali na nguvu za nje pekee; bali ni ukweli wa kiroho na wa Mwenyezi Mungu ambao hatimaye hubadilisha mwelekeo wa historia. Bibi Zaynab (s.a), akiwa na roho hii, aliuweka juu na kuendelea kubeba bendera ya haki na Uimamu katika mojawapo ya vipindi vya giza zaidi vya historia ya Uislamu.”

Mjumbe wa Mafakihi wa Baraza la Walinzi wa Katiba, akisisitiza umuhimu wa Hawza na wanazuoni wa dini kujifunza kutokana na mwenendo huu, alisema: “Hii ndiyo njia ambayo Hawza na wanazuoni wa dini wanapaswa kuifuata; yaani, hata katika mazingira magumu zaidi, waendelee kuwa na matumaini, uelewa wa kina, ushujaa na kutegemea ukweli wa Mwenyezi Mungu, ili wasiruhusu njia ya haki kusita.”

5. Katiba ya kulinda Uimamu na kuendeleza njia ya kweli ya Utume

Ayatullah Arafi, akiendelea na maelezo yake, alitaja mojawapo ya sifa muhimu zaidi za Khutba ya Fadakiyya kuwa ni nafasi yake ya kihistoria katika kulinda njia ya Uimamu na kuendeleza Utume wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w). Alisema: “Sifa ya tano ya Khutba ya Fadakiyya ni kwamba khutba hii ni katiba ya kulinda Uimamu na kuendeleza njia ya kweli ya Utume katika kipindi cha kihistoria ambacho kulikuwa na hofu kuwa njia ya Uimamu na mwendelezo halisi wa Utume vingezimika.”

Aliongeza: “Bibi Fatimah Zahraa (s.a) hakuwa akizungumza kwa ajili ya mazingira na watu wa zama zake pekee, bali kwa kutoa khutba hii aliacha ukweli muhimu kwa ajili ya mustakabali wa historia ya Uislamu pia. Lengo lilikuwa kwamba, hata kama katika kipindi hicho haikuwezekana kutimiza kikamilifu malengo yaliyokusudiwa, angalau njia ya haki isipotee na vizazi vitakavyokuja baadaye viweze kuitambua njia sahihi.”

Mkuu wa Hawza alisema: “Mafanikio ya hatua hii ya kihistoria yanaweza kuonekana katika kuendelea kuwepo na kuwa hai kwa njia hii kwa zaidi ya miaka elfu moja. Leo, baada ya kupita karne nyingi, madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s) bado yako hai, na kila mwaka tunashuhudia kuenea zaidi maarifa na mafundisho yake katika maeneo mbalimbali ya dunia.”

Kuenea maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s) duniani: Mafanikio makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu na Hawza ya Qum

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza, akizungumzia mabadiliko makubwa yaliyotokea katika uwanja wa kueneza maarifa ya Kiislamu na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s) duniani, alisema: “Leo, tunapotazama hali ya uwepo na kuenea maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s) katika nchi mbalimbali, tunakutana na mazingira ambayo hayakuwahi kushuhudiwa hapo awali. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, katika Hawza ya Qum kulikuwa na idadi ndogo tu ya wanafunzi wa elimu za kidini kutoka nchi mbalimbali, na hali ilikuwa hivyo hivyo katika mji wa Najaf. Lakini leo hali imebadilika kwa kiwango kikubwa.”

Ayatullah Arafi, akizungumzia majukumu ya kimataifa ya Hawza, alisema: “Sehemu ya majukumu na wajibu wangu wa sasa pia inahusiana na shughuli za kimataifa za Hawza. Wakati mwingine huenda kukawa na swali kuhusu uhusiano uliopo kati ya shughuli za kimataifa na Hawza. Hata hivyo, ninaamini kuwa shughuli hizi zina uhusiano wa kina na wa moja kwa moja na jukumu la Hawza.”

Aliendelea kusema: “Kwa baraka za Hawza ya Qum, wanazuoni wakubwa wa dini, Imam Khomeini (r.a), Mapinduzi ya Kiislamu na mashahidi wa njia hii, mabadiliko makubwa yamefanyika katika uwanja wa kuitambulisha na kueneza maarifa ya Uislamu na Ahlul-Bayt (a.s) duniani.

“Leo, tunapozuru baadhi ya vituo vya kimataifa, tunashuhudia idadi kubwa ya wanafunzi wa Hawza na wanazuoni wa dini kutoka nchi mbalimbali wakiwa katika vituo hivyo, wakisoma na kufanya shughuli za kielimu huku wakiwa wamehifadhi utambulisho wao wa Hawza na mavazi yao ya kitamaduni ya wanafunzi wa elimu za kidini.”

Mkuu huyo wa Hawza, akizungumzia pia kuenea maadhimisho ya Ashura ya Imam Hussein (a.s) duniani, alisema: “Leo, maadhimisho ya Ashura na shughuli za kuomboleza kwa ajili ya Sayyidush-Shuhadaa (a.s) yanafanyika kwa utukufu mkubwa katika zaidi ya nchi mia moja duniani. Bendera na kaulimbiu za Ashura zinapeperushwa katika maeneo mbalimbali ya dunia, ilhali kiwango hiki cha kuenea kwa uwepo na maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s) hakikuwahi kushuhudiwa katika zama zilizopita.”

6. Kufafanua vipengele vya kijamii, kisaikolojia na kisiasa vya jamii

Ayatullah Arafi, akifafanua sifa ya sita ya Khutba ya Fadakiyya, alisema: “Ikiwa mtu atataka kuichambua khutba hii kwa mtazamo wa elimu ya jamii, saikolojia ya kijamii na sayansi ya siasa, atabaini kuwa Bibi Fatimah Zahraa (s.a), katika khutba hii, aliichambua jamii ya Madina pamoja na mabadiliko na mazingira yaliyojitokeza ndani yake baada ya kufariki dunia Mtume Mtukufu (s.a.w.w), kwa umakini na kina kikubwa sana.”

Aliongeza: “Sisi tunaamini kuwa Ahlul-Bayt (a.s) wameunganishwa na hazina za elimu ya Mwenyezi Mungu na vyanzo halisi vya maarifa, na wana elimu na uelewa wa pekee. Hata hivyo, hata kama mtu atataka kuichunguza Khutba ya Fadakiyya kwa kutumia vigezo vya kawaida vya sayansi za kibinadamu, bila kuzingatia misingi hii ya kiitikadi, bado atatambua uwezo mkubwa wa Bibi Fatimah Zahraa (s.a) katika kufanya uchambuzi wa kijamii, kisaikolojia na kisiasa, pamoja na kutambua hali halisi ya jamii ya Madina.”

Mkuu wa Hawza nchini Iran, alisema: “Khutba hii inaweza kuchunguzwa kwa mitazamo mbalimbali ya kiitikadi, kihistoria, kijamii na kisiasa. Sifa sita muhimu tulizozitaja zinaonesha kuwa Khutba ya Fadakiyya si hotuba ya kihistoria au uwasilishaji wa madai fulani tu, bali ni katiba pana ya kufafanua ukweli, kulinda Uimamu, kuendeleza Utume na kuchambua mabadiliko yaliyotokea katika jamii ya Kiislamu.”

Mfumo wa fikra za Uislamu kuhusu neema katika sehemu mbili za mwanzo za Khutba ya Fadakiyya

Ayatullah Arafi, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alichambua baadhi ya vifungu vya mwanzo vya Khutba ya Fadakiyya. Akizungumzia namna Bibi Fatimah Zahraa (s.a) alivyoingia katika Msikiti wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w), alisema: “Bibi Zahraa (s.a) alijitokeza msikitini katika mazingira nyeti sana, akiwa na ushujaa na kujitolea kwa hali ya juu, kisha akaanza kutoa hotuba yake. Kwa mujibu wa mapokezi ya kihistoria, mkusanyiko wa watu uliathiriwa na uwepo na maneno yake katika hatua mbili, na hali ya msikiti ikabadilika.”

Aliongeza: “Hatua ya kwanza ilikuwa pale Bibi Zahraa (s.a) alipoutikisa mkusanyiko huo kwa kilio kilichotokana na kina cha msiba na huzuni aliyokuwa nayo. Kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, watu waliokuwepo walipatwa na hofu na kuguswa sana waliposikia kilio na maombolezo yake. Sauti za vilio na maombolezo zilisikika katika mkusanyiko huo, kiasi kwamba hali ya kikao iliendelea kuathiriwa na tukio hilo kwa dakika kadhaa.”

Mkuu wa Hawza aliendelea kusema: “Baada ya hapo, mazingira ya mkusanyiko yalipotulia, Bibi Fatimah Zahraa (s.a) alianza hotuba yake kwa kumhimidi na kumsifu Mwenyezi Mungu, pamoja na kumtakia rehema na amani baba yake mpendwa, Mtume Mtukufu (s.a.w.w). Sehemu hii ya khutba nayo iliamsha kumbukumbu na hisia za watu waliokuwepo, na kwa mara nyingine mkusanyiko huo ulijaa vilio na huzuni.

“Baada ya vifungu hivyo, Bibi Zahraa (s.a) aliendelea na kumhimidi na kumsifu Mwenyezi Mungu, na katika mistari ya mwanzo kabisa ya khutba yake alieleza mkusanyiko wa maarifa ya kina kuhusu neema za Mwenyezi Mungu na uhusiano wa mwanadamu na Mola wake.”

Mistari miwili ya mwanzo ya Khutba ya Fadakiyya: Kuchora mfumo wa maarifa wa Uislamu kuhusu neema

Ayatullah Arafi, akizungumzia kauli ya Bibi Fatimah Zahraa (s.a): «الْحَمْدُ لِلَّهِ عَلَی مَا أَنْعَمَ» (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu kwa neema alizozitoa), alisema: “Bibi Fatimah Zahraa (s.a), katika vifungu hivi vya mwanzo kabisa, anachora mfumo wa fikra za Uislamu kuhusu neema. Ingawa inawezekana kupata nukta na maarifa mengi zaidi kutokana na maneno haya, lakini angalau sifa kumi za msingi kuhusu neema za Mwenyezi Mungu zinaweza kutambuliwa katika sehemu hii ya khutba.”

Aliongeza: “Sifa hizi kumi zinaonesha kuwa mtazamo wa Uislamu kuhusu neema hauishii katika mali na vipawa vinavyoonekana kwa macho, bali katika mfumo wa maarifa wa Uislamu, neema ni ukweli mpana, endelevu na usio na mipaka, unaohusiana na kumhimidi Mwenyezi Mungu, Tauhidi, Wilaya na wajibu wa kijamii wa mwanadamu.”

Sifa kumi za mtazamo wa Uislamu kuhusu neema

Sifa ya kwanza: Neema za Mwenyezi Mungu zinajumuisha kila kitu katika ulimwengu

Mkuu wa Hawza aliitaja sifa ya kwanza ya neema za Mwenyezi Mungu kuwa ni kuenea kwake katika kila kitu, akisema: “Neema za Mwenyezi Mungu zinajumuisha ulimwengu wote na kila kipengele cha uwepo wa mwanadamu. Fadhila za Mwenyezi Mungu hazihusu sehemu fulani tu ya maisha au baadhi ya viumbe, bali uwepo wenyewe na daraja zote pamoja na vipengele mbalimbali vya uwepo wa mwanadamu na ulimwengu ni ishara ya huruma na neema za Mwenyezi Mungu.”

Aliongeza: “Mwenyezi Mungu amevipa viumbe vyote neema ya uwepo, na pia katika kuendeleza maisha yao amevijaalia neema mbalimbali. Kwa hiyo, kuanzia mwanzo hadi mwisho wa ulimwengu, kila kilichopo ndani yake kinategemea fadhila na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Huu ndio upana na ujumla wa neema za Mwenyezi Mungu.”

Sifa ya pili: Neema za Mwenyezi Mungu hutolewa kwa kuanzia kwake Yeye, bila ya mwanadamu kuwa na haki ya kuzistahiki

Ayatullah Arafi alitaja sifa ya pili ya neema za Mwenyezi Mungu kuwa ni kutolewa kwake kwa kuanzia kwake Yeye mwenyewe, akisema: “Neema nyingi ambazo Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu hazijatokana na kustahiki kwake wala madai yake. Hii ni kwa sababu kabla ya kupokea neema hizo, mwanadamu hana haki yoyote juu ya Mwenyezi Mungu ambayo anaweza kuitumia kudai apewe neema hizo.”

Aliendelea kusema: “Katika mahusiano ya kibinadamu, wakati mwingine mtu humfanyia mwingine wema kwa sababu mtu huyo amemuomba au amestahiki kupata wema huo. Lakini sehemu kubwa ya neema za Mwenyezi Mungu si hivyo. Neema nyingi zilizopo katika maisha yetu binafsi na ya kijamii tumepewa na Mwenyezi Mungu bila ya sisi kuziomba, na hata bila ya sisi kujua kuwa tunazihitaji.”

Mkuu huyo wa Hawza alibainisha: “Kile ambacho mwanadamu anamuomba Mwenyezi Mungu ni kidogo sana kikilinganishwa na jumla ya neema ambazo Mwenyezi Mungu amempa. Sehemu kubwa ya muundo wa maisha ya mwanadamu na mfumo wa ulimwengu imeumbwa na kuendelea kuwepo bila ya sisi kuomba au kudai.”

Sifa ya tatu: Wingi na upatikanaji mkubwa wa neema za Mwenyezi Mungu

Alitaja sifa ya tatu kuwa ni wingi na upana wa neema za Mwenyezi Mungu, akisema: “Neema za Mwenyezi Mungu zimewekwa mbele ya mwanadamu kwa wingi na kwa kiwango kikubwa. Sehemu kubwa ya uwezo na vipawa vya maisha vinapatikana kwa mwanadamu bila ya yeye kufanya juhudi maalumu na za kujitegemea ili kuvipata.”

Ayatullah Arafi aliongeza: “Mwanadamu akiitazama kwa makini maisha yake na uwezo alionao, atatambua ni kwa kiwango gani neema za Mwenyezi Mungu zimewekwa mbele yake kwa wingi na kwa upana. Ni neema ambazo nyingi zimekuwa sehemu ya kawaida ya maisha yake kiasi kwamba wakati mwingine husahau kuzingatia ukubwa na thamani yake.”

Sifa ya nne: Kuendelea na kudumu neema za Mwenyezi Mungu

Mkuu wa Hawza aliitaja sifa ya nne ya neema za Mwenyezi Mungu kuwa ni kuendelea na kudumu kwake, akisema: “Neema ya Mwenyezi Mungu haikutolewa kwa mwanadamu mara moja tu kiasi cha kufikiri kuwa baada ya hapo mambo yote yanaendelea yenyewe bila ya kutegemea chochote. Bali fadhila za Mwenyezi Mungu zinaendelea kutiririka ulimwenguni daima, kila wakati na kila sekunde.”

 Akizungumzia mijadala ya kielimu ya itikadi na falsafa kuhusu kuendelea kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, aliongeza: “Baadhi ya mitazamo imewasilishwa kana kwamba Mwenyezi Mungu aliumba ulimwengu mwanzoni, kisha ulimwengu ukaendelea na safari yake wenyewe bila ya kumtegemea tena. Lakini kwa mtazamo wa Tauhidi, fikra hiyo si sahihi. Ulimwengu katika kila sekunde unategemea fadhila za Mwenyezi Mungu, na viumbe katika kila wakati hupokea uwepo wao na uwezo wa kuendelea kuwepo kutoka Kwake.”

Ayatullah Arafi, akitumia mfano kufafanua suala hili, alisema: “Kama vile kifaa kinavyohitaji kupokea nishati mfululizo kutoka katika chanzo chake cha nishati ili kiweze kuendelea kufanya kazi, ndivyo ulimwengu mzima unavyotegemea chanzo cha fadhila za Mwenyezi Mungu katika kila wakati. Kwa hiyo, mwanadamu daima anapokea neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hakuna hata sekunde moja ya maisha yake inayojitegemea bila ya fadhila hizo.”

Sifa ya tano: Kutokuwa na mipaka na upana usio na kikomo wa neema za Mwenyezi Mungu

Alitaja sifa ya tano ya neema za Mwenyezi Mungu kuwa ni kutokuwa na mipaka kwake, akisema: “Neema za Mwenyezi Mungu zimeenea na ni nyingi kiasi kwamba hata katika ulimwengu wa vitu vinavyoonekana, mwanadamu hawezi kufikia na kuzifahamu kikamilifu nyanja na upana wake wote.”

Aliongeza: “Kile ambacho mwanadamu anakifahamu kuhusu upana wa ulimwengu wa vitu vinavyoonekana ni sehemu ndogo tu ya ukubwa wa uumbaji. Katika mfumo wa maarifa ya kidini, pia kunaelezwa kuhusu mbingu nyingine na ulimwengu ulio nje ya huu tunaoujua. Kwa hiyo, upana wa neema za Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi kuliko kile ambacho mwanadamu anaweza kukifahamu au kukizunguka kwa elimu yake yenye mipaka.”

Sifa ya sita: Mwanadamu hana uwezo wa kuzijua na kuzihesabu neema zote za Mwenyezi Mungu

Ayatullah Arafi alitaja sifa ya sita ya neema za Mwenyezi Mungu kuwa ni ugumu na kutokuwa na uwezo kwa mwanadamu wa kuzitambua na kuzihesabu zote, akisema: “Neema za Mwenyezi Mungu hazina mipaka kwa kiwango ambacho mwanadamu hawezi kuzielewa, kuzitambua na kuzihesabu zote. Mwanadamu anazifahamu sehemu ndogo tu ya neema alizopokea katika maisha yake, na hajui kuhusu neema nyingi, athari zake na vipengele vyake mbalimbali. Inawezekana kabisa kuwa katika maisha ya mwanadamu kuna neema ambazo hata hazitambui uwepo wake, au hafahamu ipasavyo thamani na umuhimu wake.”

Mkuu wa Hawza alibainisha: “Kwa sababu hiyo, mwanadamu hana uwezo wa kuzifahamu kikamilifu neema za Mwenyezi Mungu. Kadiri maarifa ya mwanadamu kuhusu Mwenyezi Mungu na ulimwengu yanavyoongezeka, ndivyo anavyozidi kutambua vipengele vingi zaidi vya upana na ukubwa wa neema za Mwenyezi Mungu.”

Sifa ya saba: Mwanadamu hana uwezo wa kulipa na kutekeleza haki ya neema za Mwenyezi Mungu

Mkuu huyo wa Hawza alitaja sifa ya saba kuwa ni kutokuwa na uwezo wa kulipa kikamilifu neema za Mwenyezi Mungu, akisema: “Mwanadamu hawezi kamwe kutekeleza kikamilifu haki ya neema za Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu hata kama angependa kutoa malipo fulani kama fidia ya neema alizopewa na Mwenyezi Mungu, uwezo wenyewe wa kufanya hivyo pia ni miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu.”

Ayatullah Arafi aliongeza: “Kwa mfano, mtu akimzawadia mwingine kitabu, inawezekana mtu huyo akamnunulia zawadi nyingine na kumpa kama malipo ya zawadi aliyopokea. Lakini hali si hivyo katika neema za Mwenyezi Mungu. Juhudi zote ambazo mwanadamu anazifanya katika njia ya kushukuru na kumuabudu Mwenyezi Mungu, hata nyenzo, uwezo na fursa za kufanya hivyo, vyote amepewa na Mwenyezi Mungu.”

Akizungumzia ukweli kwamba hata kitendo cha mwanadamu cha kushukuru kinategemea fadhila za Mwenyezi Mungu, alisema:b“Mwanadamu hawezi kudai kuwa kwa ibada au shukrani zake ametekeleza haki ya neema za Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu hata ibada na shukrani hizo ni tawfiki kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na haziwezi kuchukuliwa kuwa ni malipo yanayolingana na neema Zake zisizo na mwisho.”

Sifa ya nane: Kuongezeka neema kupitia shukrani na kupanda daraja ya kiroho ya mwanadamu

Mkuu wa Hawza aliitaja sifa ya nane ya neema za Mwenyezi Mungu kuwa ni uhusiano wa shukrani na kuongezeka kwa neema pamoja na kupanda daraja ya kiroho ya mwanadamu, akisema:b“Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an Tukufu: لَئِنْ شَکَرْتُمْ لَأَزِیدَنَّکُمْ; ‘Hakika mkishukuru, nitawazidishia neema Zangu.’”

Akisisitiza kuwa maana ya kuongezeka neema haipaswi kufungwa katika kupata mali na vitu vingi zaidi, aliongeza: “Wakati mwingine watu hufikiri kuwa mwanadamu akimshukuru Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu atampa neema nyingine kama mali, uwezo au maisha ya starehe zaidi. Hata hivyo, mojawapo ya maana muhimu zaidi za aya hii ni kwamba kitendo chenyewe cha kushukuru kinakuwa sababu ya kukua na kuimarika kwa uwepo wa mwanadamu.”

Ayatullah Arafi aliendelea kusema: “Mwanadamu anaposwali, kumhimidi Mwenyezi Mungu au kujiweka katika njia ya ibada na utumwa Kwake, hapaswi kusubiri tu kupata malipo fulani baadaye. Bali ibada na shukrani hizo zenyewe zinakuwa sababu ya ukuaji wake wa kiroho na kupanda kwa daraja yake.”

Akizungumzia pia nafasi ya subira, uvumilivu na kumtegemea Mwenyezi Mungu wakati wa kukabiliana na matatizo, alisema: “Mwanadamu anapokumbwa na msiba, akasubiri mbele ya matatizo, akayavumilia na kumtegemea Mwenyezi Mungu, hapaswi kulitazama suala hilo kwa mtazamo wa kupata fidia ya mali au mambo ya nje pekee. Miongoni mwa athari muhimu zaidi za subira na uvumilivu huo ni kupanda kwa daraja ya kiroho ya mwanadamu mwenyewe.”

Mkuu huyo wa Hawza alihitimisha kwa kusema: “Kwa hiyo, shukrani, subira na kumtegemea Mwenyezi Mungu si hatua za awali za kupata malipo ya nje tu, bali vyenyewe ni sababu za kukamilika na kukua mwanadamu.”

Sifa ya tisa: Uhusiano wa kweli kati ya neema za Mwenyezi Mungu na kumhimidi Yeye, Tauhidi, Utume na Wilaya

Ayatullah Arafi, akifafanua sifa ya tisa ya neema za Mwenyezi Mungu, alizungumzia uhusiano wa kina uliopo kati ya neema na kumhimidi na kumsifu Mwenyezi Mungu, pamoja na maarifa ya Tauhidi na Wilaya. Alisema: “Jambo muhimu sana ni kwamba neema za Mwenyezi Mungu hazipaswi kutenganishwa na ukweli wa kumhimidi na kumsifu Yeye. Mwenyezi Mungu humpa mwanadamu neema, na kwa upande mwingine anamtaka awe mwenye kumhimidi na kumshukuru. Hata hivyo, uhusiano huu si makubaliano ya kawaida tu wala si mambo mawili yaliyojitenga.”

Akizungumzia aya tukufu isemayo: «الْیَوْمَ أَکْمَلْتُ لَکُمْ دِینَکُمْ وَ أَتْمَمْتُ عَلَیْکُمْ نِعْمَتِی» (Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimeitimiza neema Yangu juu yenu), alisema: “Kukamilishwa dini na kutimizwa kwa neema katika aya hii ni ukweli wenye kina na unaohusiana kwa karibu. Uhusiano kati ya neema ya Mwenyezi Mungu, Tauhidi, Utume na Wilaya si uhusiano wa kuunganisha tu mambo kadhaa yanayojitegemea, bali vipengele hivi vimeunganishwa katika ukweli na asili ya neema ya Mwenyezi Mungu.”

Mkuu wa Hawza aliongeza kusema: “Neema kama umri, ujana, afya, fursa ya kusoma, tawfiki ya kufundisha, shughuli za kielimu na kijamii pamoja na mahitaji ya maisha, hupata njia yake ya kweli pale ambapo kumhimidi na kumsifu Mwenyezi Mungu, Tauhidi, Utume na Wilaya vinapokuwa ndio vinavyovitawala.”

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Elimu za Kiislamu alisisitiza: “Ikiwa ukweli huu hautakuwepo katika maisha ya mwanadamu, inawezekana akawa na mali na uwezo mwingi wa kidunia, lakini akawa mbali na ukweli na ukamilifu halisi wa neema. Katika mfumo wa maarifa ya Uislamu, neema hupata maana yake na ukamilifu wake wa kweli kupitia kumwabudu Mwenyezi Mungu na kujiweka katika njia ya Tauhidi na Wilaya.”

Sifa ya kumi: Kuigeuza neema kuwa huduma kwa jamii na kuwafanyia wengine wema

Ayatullah Arafi alitaja sifa ya kumi ya neema za Mwenyezi Mungu kuwa ni uhusiano wake na wajibu wa kijamii pamoja na kuwahudumia wengine. Alisema: “Ukweli wa kushukuru neema hauishii katika mwanadamu kusema kwa ulimi wake kuwa namshukuru Mwenyezi Mungu. Bali shukrani ya kweli hutimia pale mwanadamu anapotumia neema alizopewa na Mwenyezi Mungu katika njia ya kuwahudumia wengine.”

Aliongeza: “Mwenyezi Mungu amemfanyia mwanadamu wema, hivyo mwanadamu naye anapaswa kuwafanyia wengine wema. Mwenyezi Mungu amemruzuku mwanadamu, hivyo mwanadamu naye anapaswa kuchukua hatua katika kuwapa chakula na kuwasaidia wenye mahitaji. Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu mwongozo na uongofu, hivyo mwanadamu naye anapaswa kuwaongoza wengine.”

Mkuu wa Hawza akisisitiza kuwa kuiga fadhila na wema wa Mwenyezi Mungu kunapaswa kudhihirika katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii, alisema: “Ikiwa Mwenyezi Mungu amemshika mkono mwanadamu na kumuongoza, basi mwanadamu naye anapaswa kuwashika mikono wengine. Ikiwa Mwenyezi Mungu amempa uwezo na fursa mbalimbali, basi anapaswa kuzitumia katika njia ya kheri na kuwahudumia wanajamii.”

Mjumbe wa Mafakihi wa Baraza la Walinzi wa Katiba aliendelea kusema: “Mtazamo huu ndio roho inayopaswa kutawala mahusiano ya kijamii na maisha ya mtu binafsi na ya pamoja. Mwanadamu anapaswa kujifunza kutoka kwa Mwenyezi Mungu namna ya kufanya wema, kuwasaidia wengine, kuwahudumia wenye mahitaji na kutumia alichonacho kwa ajili ya ukuaji na maendeleo ya wengine.”

Ayatullah Arafi, akiendelea na maelezo yake, alisisitiza: “Vifungu viwili vya mwanzo vya Khutba ya Fadakiyya vinamweka mwanadamu mbele ya mfumo mpana wa fikra za Kiislamu kuhusu neema. Ni mfumo ambao huanzia katika fadhila za Mwenyezi Mungu zilizoenea kila mahali na zinazoendelea daima, hukamilika kupitia kumhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu, Tauhidi na Wilaya, na hatimaye hujitokeza katika maisha ya kijamii ya mwanadamu kupitia kufanya wema, kutoa huduma na kuwashika mikono wengine.”

Utambulisho wa Hawza ni kufufua ukweli wa Tauhidi na hali ya kiroho katika jamii za wanadamu

Ayatullah Alireza Arafi, akisisitiza nafasi na utambulisho wa kistaarabu wa Hawza za Elimu za Kiislamu, alisema: “Utambulisho wa Hawza unafafanuliwa katika njia hii na jukumu hili ambalo tunapaswa kulipokea kutoka katika Hawza na kulifanya liwe sehemu ya maisha ya mtu binafsi na ya kijamii ya mwanadamu. Leo, jamii za wanadamu zinahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuwasilishwa ukweli wa Mwenyezi Mungu, ili ukweli huo uweze kutangazwa duniani na kuyapa maisha ya wanadamu uhai.”

Mjumbe wa Mafakihi wa Baraza la Walinzi wa Katiba aliongeza: “Mwanafunzi wa elimu za kidini na Hawza, wanapaswa kuwapo ndani ya maisha halisi ya jamii za wanadamu na kuyapa maisha ya mwanadamu utambulisho. Jukumu la Hawza ni kuingiza ukweli wa Tauhidi, Utume, Wilaya na vipengele vya ibada na kiroho vya dini katika mabadiliko yote ya maisha ya mwanadamu. Hii ni kwa sababu ikiwa ukweli huu hautakuwepo katika maisha ya mwanadamu, basi uwezo na neema zote za ulimwengu huu, licha ya thamani na umuhimu wake wa nje, zitakosa ukweli na maana yake halisi.”

Jukumu la mwanafunzi wa elimu za kidini ni wajibu mkubwa na unaoamua mustakabali

Mkuu wa Hawza, akizungumzia umuhimu wa nafasi ya mwanafunzi wa elimu za kidini na wajibu mkubwa ulio mabegani mwa wanafunzi hao, alisema: “Kazi mliyoibeba ni kubwa mno na yenye thamani kubwa, hivyo haipaswi kuichukulia kijuujuu wala kuiona kuwa ni jambo dogo. Hasa katika umri wa ujana, ambapo ndani yenu kuna uwezo, vipaji na vipawa vingi sana vilivyofichika, ambavyo mnapaswa kuvikuza kupitia usimamizi na mipango mizuri.”

Akisisitiza umuhimu wa wanafunzi kujiamini na kuwajibika, alisema: “Msisubiri viongozi, walimu na watu wengine ndio wawatengezee mazingira ya kukua na kupiga hatua. Bila shaka, mwanafunzi wa elimu za kidini anapaswa kutumia uwezo wote wa kielimu, kimalezi na kimafunzo wa walimu na wanazuoni wakubwa. Lakini hatimaye, yeye mwenyewe anapaswa kuwa mhandisi wa kujijenga kwake, mbunifu wa nafsi yake, mjenzi wa mustakabali wake na mjenzi wa mustakabali wa jamii.”

Ayatullah Arafi aliendelea kusema: “Mwanafunzi wa elimu ya dini anapaswa kufahamu kuwa ameingia katika njia ambayo inahusiana na elimu tukufu zaidi na mojawapo ya njia bora kabisa ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuwekea mwanadamu. Fursa hii na mtaji huu wa Mwenyezi Mungu vinapaswa kuthaminiwa, na mtu anapaswa kutumia uwezo wake wote ili kufikia kilele cha elimu, maadili na ukamilifu wa kiroho.”

Thamani ya ndani ya mwanazuoni wa dini ni kubwa kuliko mali yoyote ya kidunia

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza, akizungumzia thamani na heshima ya wanazuoni wa dini pamoja na nafasi yao ya kiroho, alisema: “Thamani ya ndani ya mwanazuoni wa dini na mtaji huu safi na wenye thamani kubwa haupaswi kubadilishwa kwa mambo ya kimwili na bidhaa za kidunia. Thamani na heshima ya mwanazuoni wa dini viko juu ya kila kitu, na nafasi hii inapaswa kufahamika na kuhifadhiwa ipasavyo.”

Mkuu wa Hawza, akisisitiza umuhimu wa kuwalea wanafunzi wa elimu ya dini katika nyanja zote, alisema: “Kuhifadhi nafasi hii yenye thamani kubwa kunahitaji malezi sahihi, maarifa sahihi, uelewa wa kina na kujiweka katika njia ya kuitumikia dini. Mwanafunzi wa elimu ya dini anapaswa, kwa kufahamu kwa usahihi wajibu wake na kuwa na mtazamo pamoja na uelewa unaohitajika, kuulinda mtaji huu wenye thamani kubwa na kuutumia katika kuiinua dini na jamii.”

Mabilioni ya wanadamu wa leo na vizazi vijavyo ndio walengwa wa ujumbe wa wanafunzi wa Hawza

Ayatullah Arafi, akizungumzia upana wa kimataifa wa majukumu ya Hawza na wanafunzi wake, alisema:v“Hii ndiyo njia ambayo tunapaswa kujifunza kuifahamu kwa usahihi na kuifuata kwa uelewa na utambuzi. Sisi sote, kuanzia viongozi na walimu hadi wale wanaoshiriki katika shughuli za elimu na malezi, ni watumishi ambao tunapaswa kuweka mazingira ya malezi yenu ili ninyi muweze kujenga mustakabali wa Hawza, nchi, mfumo wa utawala, Mapinduzi ya Kiislamu na hata ulimwengu mzima.”

Mjumbe wa Mafakihi wa Baraza la Walinzi wa Katiba, akisisitiza kuwa; jukumu la wanafunzi wa elimu ya dini halina mipaka ya eneo au jamii fulani, alisema: “Wanadamu wote duniani ndio walengwa wa ujumbe na jukumu lenu. Leo, kuna idadi ya watu wapatao bilioni saba hadi nane wanaoishi duniani. Zaidi ya hapo, mabilioni ya wanadamu watakaoishi katika vizazi vijavyo nao ni walengwa wa ujumbe na jukumu lenu la kielimu, kidini na la kueneza mafundisho ya dini.”

Mkuu wa Hawza aliendelea kusema: “Mimi daima nimekuwa nikiwakumbusha marafiki zetu katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa (s.a) kuwa watu bilioni saba waliopo duniani leo, pamoja na mabilioni ya watu watakaokuja katika vizazi vijavyo, ndio walengwa wa ujumbe wenu. Huu ni wajibu mkubwa sana unaohitaji maandalizi yanayolingana na ukubwa wake.”

Masharti ya kutekeleza jukumu la kimataifa la wanafunzi wa Hawza

Ayatullah Arafi, akihitimisha hotuba yake kwa kutaja sifa zinazohitajika ili kutekeleza jukumu hili kubwa, alisema: “Kutekeleza jukumu la aina hii kunahitaji elimu, maadili mema, uelewa wa kina, maarifa, mtazamo mpana, moyo mpana kama bahari na imani thabiti. Mnapaswa kujipatia hazina hizi ndani ya nafsi zenu, na kwa kuimarisha misingi yenu ya kielimu, kimaadili na kiitikadi, mujiandae kukabiliana na mahitaji ya kimawazo na kiroho ya wanadamu wote.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha